Drone Online

KARIBU YAKO KWA HABARI ZA UHAKIKA,MAKALA,MICHEZO,MITINDO YA MAISHA NA BURUDANI

Post Page Advertisement [Top]

 


Jijini Dar es Salaam. Sakata la Jaji Mkuu, Profesa Ibrahimu Juma kuendelea kusalia kwenye nafasi hiyo limechukua sura mpya baada ya Wakili wa kujitegemea, Humphrey Simon Malenga kufungua kesi ya kikatiba Mahakama Kuu Masjala Kuu, Dar es Salaam kupinga kiongozi huyo kuongezewa muda wa utumishi huo.


Malenga amefungua kesi hiyo siku chache baada ya Jaji wa Mahakama ya Rufani, Stella Mugasha kumwandikia barua Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Profesa Elisante Ole Gabriel kupinga uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kumuongezea muda Profesa Juma.


Profesa Juma, ambaye alizaliwa Juni 15, 1958, amekuwa Jaji Mkuu wa Tanzania kuanzia Septemba 10, 2017, mara baada ya kuteuliwa na kuapishwa na Rais wa wakati huo, John Magufuli akichukua nafasi ya Mohamed Othuman Chande aliyestaafu.


Juni 15, 2023, Profesa Juma alitimiza miaka 65 ambayo kwa mujibu wa Katiba inamfanya kustaafu.


Hata hivyo, Rais Samia alimwongezea muda wa kuendelea na utumishi katika nafasi hiyo kwa mua ambao bado haujawekwa wazi.


Katika shauri hilo namba 7 la mwaka 2023, dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Malenga anaiomba mahakama itoe tafsiri ya ibara za Katiba kuhusiana na mamlaka ya Rais kuahirisha au kuongeza umri wa kustaafu wa utumishi wa Jaji Mkuu.


Ibara hizo ambazo Malenga anaiomba mahakama hiyo izitolee tafsiri ni ibara ya 118(2) na 120 (2) na (3).


Ibara ya 118(2) inaeleza Jaji Mkuu ambaye ni mkuu wa Mahakama ya Rufani na wa Mhimili wa Mahakama kwa ujumla atatumikia wadhifa huo mpaka atakapotimiza umri wa kustaafu wa Jaji wa Mahakama ya Rufani.


Ibara ya 120 (2) na (3) ibainisha umri wa kustaafu wa Jaji wa Mahakama wa Rufani ni miaka 65, lakini inabainisha kuwa Rais akiona inafaa anaweza kumuongezea muda maalumu mpaka mwisho wa muda huo wa nyongeza utakapoisha.


Ibara 120(4) inafafanua pia Jaji wa Mahakama ya Rufani anaweza kuendelea na majukumu yake hata baada ya kufikisha umri wa miaka 65 mpaka pale atakapokamilisha kuandaa na kutoa hukumu za mashauri kesi alizozisikiliza au shughuli au mashauri aliyokwishaanza kuyasikiliza.


Mjadala unaibuka hapa ni kama masharti ya ibara 120(2) (3) kuhusu jaji wa Mahakama ya Rufani kuongezewa muda wa utumishi na Raisi inasomwa pamoja na ibara ya 118(2), kwamba masharti hayo yanamhusu pia Jaji Mkuu au la.


Hivyo Malenga anaiomba mahakama hiyo itoe tafsiri masharti ya Ibara ya 118(2) kuhusiana na umri wa kustaafu wa Jaji Mkuu kwamba ni miaka 65 na si umri wa kustaafu wa jaji wa kawaida wa Mahakama ya Rufani.


Anaiomba pia mahakama hiyo itoe tafsiri kwamba Ibara ya 118(2) ni ibara inayosimama peke yake, haihusiani na Ibara ya 120(1), (2), (3) na (4) katika kuamua umri wa kustaafu utumishi wa Jaji Mkuu.


Vilevile Malenga anaiomba mahakama itafsiri mamlaka ya Rais kuzuia kustaafu au kumuongezea muda wa utumishi Jaji wa Mahakama ya Rufani kwa maslahi ya umma kwa mujibu wa ibara hiyo ya 120(2) na (3) hayatumiki kwa Jaji wa Mahakama ya Rufani ambaye pia ni Jaji Mkuu.


Mwisho anaiomba mahakama hiyo itamke kwamba kuahirishwa kwa uamuzi wa kustaafu au kuongezewa muda wa utumishi wa Jaji wa Mahakama ya Rufani wa sasa, ambaye pia ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Juma kwa mujibu wa Ibara ya 120(2) na au 120(3), ni kinyume cha Katiba.


Kesi ilifunguliwa mahakamani hapo Juni 28, 2023 imepangwa kusikilizwa na Jaji Godfrey Isaya na imetajwa kwa mara ya kwanza Jana Jumatatu, Julai 3, 2023 mbele ya mawakili wa pande zote.


Malenga anawakilishwa na jopo la mawakili watatu, Ipilinga Panya, Aliko Mwamanenge na Joyce Brown na Serikali iliwakilishwa na mawakili wa Serikali Alice Mturo na Bravoo Junus ambao waliomba na kuruhusiwa na mahakama kuwasilisha majibu ya Serikali ya maandishi Julai 6, 2023.

No comments:

Post a Comment

Bottom Ad [Post Page]